MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amekamatwa na polisi
eneo la viwanda (EPZA) Mabibo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul
Makonda.
Tukio hilo limetokea kukiwa na mgomo wa wafanyakazi zaidi ya
1800 wa kiwanda cha nguo cha TZ TOOKU ambao walimpigia mbunge wao aende kutatua
mgogoro huo.
Kubenea alifika katika eneo hilo saa 6 mchana, akakutana na
wafanyakazi kusikiliza kero zao za muda mrefu.
Kisha aliamua kuondoka na viongozi wa wafanyakazi hao na kufanya
kikao na menejimenti ya kiwanda hicho kuanzia saa 7 hadi saa 9.
Ilipofika saa 10:30 Makonda alikuja na kupata taarifa kwa muafaka
uliofikiwa kati ya Kubenea, menejimenti na viongozi wa wafanyakazi.
Alitoa amri wafanyakazi wakusanyike, akaawaambia kesho atafika
huko na Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Kazi na Ajira, na Waziri wa
Afya Wanawake, Jinsia na Watoto.
Baada ya kutoa maagizo hayo, Makonda alimzuia Mbunge asihutubie
kuaga wananchi aliokuwa nao tangu mchana, kutokana na hali hiyo Kubenea alisema
ni vema aseme neno, ndipo mvutano ulipoanza.
Makonda alimuru mkutano ufungwe lakini wafanyakazi
hawakutawanyika eneo hilo, alipoona hivyo aliamrisha Polisi wamkamate Kubenea,
kwa madai alimwita yeye Kibaka.
Katika tukio hilo, Mwandishi wa habari wa Star Tv aliyekuwa
anarekodi tukio hilo alinyang’anywa kamera na Polisi aliyejulikana kwa jina
moja tu la Denis.
Mwandishi wa habari Mwanahalisi alijaribu kumsaidia mwenzake ili
arejeshewe kamera lakini Polisi wa kituo cha Magomeni walimtisha, na kumtaka
kuondoka haraka huku wakiondoka na aliyenyang’anywa kamera.
Bado Kubenea anaendelea kuhojiwa na polisi katika kituo cha Magomeni
akiwa na mwanasheria wake, Fred Kihwelo
0 comments:
Post a Comment