*Wahofia kwenda na kasi ya Hapa Kazi Tu!
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WABUNGE wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
wametajwa kukataa uteuzi wa nafasi ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne
zilizokuwa wazi, MTANZANIA imebaini.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni
hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye
aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12, mwaka huu.
Wakizungumza na MTANZANIA wabunge hao ambao
hawakupenda kutajwa majina yao gazetini walidai kuwa kasi ya Rais Magufuli
inawatia hofu.
“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito na kwangu
ni ngumu na nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya taarifa hizi nasikia
na wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.
“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada ya kupima
nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge wangu,” alisema
mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
WIZARA NNE ZILIZOKOSA MAWAZIRI
Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri, Desemba 10,
mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana
na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo na kwamba anaendelea
kuwatafuta.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliteua manaibu
waziri wa wizara hizo, huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake
baadaye atakapomaliza mchakato.
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na
Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na
Mipango, ambayo naibu wake ni Dk. Ashatu Kijaji.
Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii, ambayo naibu
wake ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi
ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.
KINANA ATOBOA SIRI
Mwishoni mwa wiki akiwa mkoani Arusha, Katibu Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alitoa siri ya wabunge wanne
ambao walipigiwa simu za uteuzi wa uwaziri, lakini walikataa kwa hofu ya
kushindwa kwenda na kasi ya Rais Magufuli.
Alisema anachoamini ni kwamba Rais John Magufuli,
atakuwa aliwaeleza baadhi ya wabunge kuhusu nia yake ya kuwateua katika nafasi
hizo, lakini wao wakamwomba asiwape majukumu hayo kwa kuwa hawana uhakika wa
kwenda na kasi anayohitaji katika Serikali yake.
Kinana alisema kinachojitokeza sasa ni kama
alivyoshauri Rais Magufuli kuwa si vema kwa waziri aliyeteuliwa kufanya sherehe
nyumbani kwake na kuita marafiki kwa kuwa wana mzigo mzito katika kuwatumikia
wananchi.
“Ni vema mawaziri hawa wakafanya maombi kwa kuwaita
au kuwafuata viongozi wa dini kwani wana kazi ngumu kulingana na nia njema
aliyonayo Rais Magufuli katika kupambana na masuala ya ufisadi.
“… kazi ya kupambana na ufisadi kamwe si rahisi hadi
kushangilia uteuzi, lengo kubwa ni kuwaletea wananchi maendeleo kupitia
ubinafsishaji wa viwanda kutoka kwa watu waliomilikishwa na kuviua,” alisema
Kinana.
Katibu mkuu huyo wa CCM, alisema anaunga mkono
uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi dunaini, hali
ya kuwa wagonjwa hawana dawa.
“Nyingine ni Wiki ya Maji, mnafanya maadhimisho huku
watu hawana maji, Wiki ya Maziwa wakati wafugaji wamekonda na mifugo imekonda
haitoi maziwa, fedha hizo zitumike kwa mambo mengine,” alisema Kinana.
MIKATABA KWA MAWAZIRI
Wakati wa kampeni za kuwania urais, Dk. Magufuli,
aliahidi kama atafanikiwa kuingia madarakani, atawasainisha mikataba maalumu ya
kazi mawaziri wake kabla ya uteuzi.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha
anakuwa na mawaziri wanaokwenda kwa wananchi badala ya kukaa ofisini wakiandika
madokezo.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, atafanya hivyo kwa kuwa
anahitaji kuunda Serikali itakayokuwa na mawaziri waliotayari kulitumikia taifa
kwa uadilifu.
Kutokana na ahadi hiyo MTANZANIA ilimtafuta Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ili kujua iwapo
mawaziri walioteuliwa wamesainishwa mikataba au laa.
Katika majibu yake Msigwa alisema asingeweza
kuzungumza kwani yupo katika kikao na kuahidi kuwa atalitolea ufafanuzi suala
hilo baada ya muda.
Desemba 10, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza
Baraza la Mawaziri lenye jumla ya wizara 18 zenye mawaziri 19, huku wizara moja
ikiwa na mawaziri wawili.
Katika uteuzi huo, mawaziri 13 walikuwamo katika
Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya
Kikwete, huku wapya wakiwa wawili ambao ni Balozi Dk. Augustine Mahiga na Nape
Nnauye.
Kwa upande wa manaibu waziri, wengi ni sura mpya
ambazo hazikuwamo katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne.
Uamuzi wa kutangaza baraza hilo unavunja ukimya na
maswali ya muda mrefu kuhusu uundwaji wa baraza hilo.
Rais Magufuli, alisema pamoja na hali hiyo hata
akikamilisha uteuzi wa wizara nne zilizobaki, baraza lake la mawaziri litakuwa
na mawaziri 34 tu tofauti na Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu
Jakaya Kikwete, iliyokuwa na mawaziri 60 pamoja na manaibu.
0 comments:
Post a Comment